Tuesday, June 8, 2010

Watanzania na Ujio wa Brazil



Kipyenga cha mwisho kimelia, huku Brazil wakishinda mpambano dhidi ya Taifa Stars kwa magoli matano kwa moja. Mazungumzo na mabishano juu ya mechi hii iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na Watanzania wengi itabaki kuwa gumzo la jiji kama sio nchi, kwa wiki kadhaa zijazo. Watanzania tutaelekeza nguvu zetu kwenye kupiga domo juu ya mechi hii huko vijiweni kabla ya hali halisi ya maisha yetu duni kutuzindua kwenye starehe hii iliyo dumu kwa dakika 90.

Ujio wa Brazil umepokelewa kwa hisia tofauti, wengi wakishabikia kuwa hatimaye watamwona mchezaji mahiri wa Brazil, KaKa kwa macho yao wenyewe. Kuna kundi dogo la watu waliotaka Watanzania tususie mechi kwani haina manufaa yoyote katika kuendeleza uchumi wa nchi yetu. Zogo hili la ujio wa Brazil lilianza kupaa kwa kasi pale Bw Paulo Kamau wa Kenya alipobeza uamuzi huu wa Tanzania kuwalipa fedha nyingi vijana hao wa Samba.

Tanzania Football Federation (TFF) wamekuwa kimya kuzungumzia kiwango halisi walichowapa Brazil, wakati mwazoni walidai kuwa Serikali iliwatengea fungu la dola za Kimarekani milioni sita. Tovuti ya BBC wamedai kuwa TFF iliwalipa dola milioni mbili na nusu. Kiasi taslimu cha fedha walicholipwa Brazil bado kinabaki kuwa tata, huku Raisi wa TFF ndugu Leodegar Tenga akidai kuwa, "It's definitely that the coming of top players in the world will be a big boost to local football as well as the tourism sector,".

TFF imejitetea kuwa, ujio wa Brazil utachochea maendeleo katika soka na kwenye sekta ya utalii. Hizi ndizo sababu kuu mbili zakutetea matumizi makubwa ya fedha ya kuwalipa Brazil kuja kucheza na Taifa Stars, sasa swali ni hili, Je Tenga na TFF wana hoja ya msingi?

Mimi binafsi sidhani kama hoja hiyo ina nguvu ya kutosha kuhalalisha matumizi ya hivyo vijisenti walivyowalipa Brazil, na hoja zangu ni kama ifuatavyo. Soka la Tanzania limekuwa kichwa cha mwendawazimu kwa miaka mingi, na mimi nina uhakika wengi tunajua ni nini kinatakiwa kufanyika ili kuinua soka la Tanzania. Tatizo la kwanza, tunapenda kukimbia kabla hatujajua kutembea, na hoja hii aliizungumzia kocha wa Taifa Stars wa sasa ndugu Marcio Maximo alipotoa ushauri wake juu ya soka la Bongo. Mimi sio mtaalamu saana wa soka wala sijawahi kuwa kwenye kamati ya ufundi wa tunguli, lakini hoja ya Maximo itaungwa mkono na wengi wenye uwerevu. Watanzania inatubidi tuanze kujenga utamaduni wa kusikiliza wataalamu na sio wanasiasa wasio jua lolote.

Sasa tukija kwenye sababu ya pili, ya kuwa ujio wa Brazil utasaidia soko la utalii, nadhani kuna mambo kadhaa ya kuangalia kwa utaratibu. Jambo la kwanza, tuna uhakika gani ujio wao utaongeza ujio wa watalii? Najua moja ya jibu la swali hili litakuwa, kwasababu mechi inaonyeshwa moja moja katika nchi zisizopungua mia 160. Hii inaweza saidia; lakini wasiwasi wangu ni kuwa, kuna utafiti mdogo umefanywa katika kuhakikisha kuwa hii ndio njia bora ya kutangaza nchi yetu. Katika mpango huo, je tuliangalia njia mbadala ambazo zingetugharimu fedha kidogo zaidi na ambazo tungekuwa na uhakika zaidi kuwa zitazaa matunda?

Waziri wa Mali asili na Utalii, Mh. Shamsa Selengai Mwangunga (MB) alipotoa makadirio ya Wizara yake Bungeni, aliongelea mipango kadhaa ya Wizara yake. Moja ya mipango hiyo ilikuwa ni kuongeza utalii wa ndani, kwa kuwapunguzia Watanzania viingilio katika mbuga za wanyama na sehemu nyingine za kitalii. Mkakati huo ni mzuri, lakini bado tunategemea zaidi watalii wa nje. Lakini kidogo kimefanyika kuhamasisha watalii wa nje kuja nchini. Tanzania bado inatajwa kama nchi yenye viwango vikubwa (fees) kwa watalii, ukilinganisha na Kenya na Uganda. Kenya na Uganda walipunguza viwango vyao baada ya uchumi wa dunia kuyumba, lakini Tanzania bado tumeacha viwango vikiwa juu. Sasa hapo ndio kuna mgongano wa mawazo -- huku tunatumia mamilioni kadhaa kutangaza nchi, lakini hatupunguzi viwango. Hao watalii wataishia kwenda Kenya na Uganda na kukwepa Tanzania, hivyo mwisho wa siku tunajaza maji kwenye pekecha.

Ripoti ya Repoa iliyokuwa inazungumzia The Role of Tourism in Poverty Alleviation in Tanzania ni ripoti inayotoa mapendekezo yakinifu. Pamoja na ripoti hiyo iliyotoka miaka saba iliyopita, lakini mapendekezo yake bado yana umuhimu, sasa sijui mapendekezo mangapi ya ripoti hiyo yalifanyiwa kazi na Serikali kupitia Wizara yake husika. Mimi nakubali sekta ya utalii inaumuhimu mkubwa, hasa katika kuchangia kupunguza umasikini. Lakini je, tumeboresha sekta hiyo kwa kiasi gani? Tanzania leo tunaweza kusema huduma zetu za utalii zinaweza kushindana na nchi nyingine za Afrika au bado huduma zetu ni duni. Miundombinu bado ni tatizo kubwa, lakini tumeng’ang’ania kutangaza nchi. Jamani, akili ya namna hii haina tofauti na akili ya mtu anayekaribisha wageni kabla ya kufagia nyumba na kuhakikisha kila kitu kiko sawa.

Timu ya Brazil nd’o hiyo imekuja na kuondoka, sasa ningependa kuona kama malengo ya mpango huo yatafikiwa; soka ya bongo kuhamasika na hao watalii kuongezeka. Mimi kwa kiasi fulani ninakubaliana na baadhi ya watu waliotaka Watanzania tususie mechi hiyo na pia ninakubaliana kwa kiasi fulani na mawazo ya Kamau. Tanzania ni nchi masikini kutumbua fedha zote hizo kwenye kitu ambacho hatuna uhakika kitalipa. Tanzania tukiwa kama nchi moja masikini sana duniani, lazima tuwekeze fedha za walalahoi kwenye mambo ya msingi zaidi, sio kwenye starehe za dakika mbili tatu. Majuzi tu, tulikuwa wenyeji wa mkutano wa uchumi wa dunia. Ukiniuliza mimi hiyo ilikuwa nafasi nzuri kutangaza nchi. Je, tulifanya hivyo ipasavyo, au tulishangalia tu wageni waliokuja?

Aliyesema ng’ombe wa masikini hazai, hakukosea. Na msemo huu ni kweli kwani, ni watu masikini ambao mara nyingi hufanya maamuzi ya papara bila kufikiria kuwa kuna kesho. Tuendelee kuzungumzia ni jinsi gani Brazil walivyopigwa chenga na Taifa Stars, lakini wao haoooo wanaelekea kwenye Kombe la Dunia, Sisi je? Kamau alivyozungumzia “character” yetu Watanzania hakukosea sana. Pamoja simuungi mkono na kejeli zake, lakini alikuwa na hoja. Hivi kweli watu wazima tunaweza kusema,” tumefungwa lakini tuliwapiga chenga”. Hilo ni jambo la kushabikia kweli? Tukiendelea na akili hizo sisi kila siku tutanyonywa na kukandamizwa kwani tumekuwa watu wa kufurahia mafanikio madogo, tena ya kijinga, badala ya kusimama na kupigania maendeleo makubwa yenye maana. Tumezidi kuwa wa ndio mzee, badala ya kuuliza maswali, kupigania haki zetu na kupigani uwajibishwaji wa viongozi wabovu wenye kunuka ufisadi. Watanzania, hivi ndio tumekubali kuwa umasikini ni utamaduni wetu?

Watanzania wenzangu waliojitutumua na kulipa viwango vikubwa kuwaona Brazil, je, ulifikiria mechi hiyo kama ina manufaa kwa nchi yetu. Hivi ni wewe huyo huyo unayelalamika kuwa barabara zimechakaa na msongamano wa magari umekithiri. Wewe ulilipa kwenda kumwangalia KaKa, je nyumbani kwako haupatagi matatizo ya kukatiwa maji na umeme mara kwa mara au unajenerata na bwana la maji nyumbani? Leo hii ukalipe fedha zote hizo kuwaona Brazil, alafu kesho unafanya kila uwezalo kukwepa kulipa kodi na kupokea rushwa. Watanzania tunazungumzia sana kuhusu tulivyo masikini, lakini hapo hapo tunataka starehe zinazotushinda uwezo. Naona tunataka kulazimisha maji yachanganyike na mafuta; kweli Tanzania tuna akili zinazotutosha sisi wenyewe.

Ushauri wangu ni huu, kama tulivyopigania tiketi za kumwona KaKa, basi moyo huo huo wa kupigana usiishie hapo. Moyo huo uendelee katika kupigania maendeleo, kupinga viongozi wabovu, tuwe na kiu ya maendeleo na ari ya kuchapa kazi kama tulivyoshangilia magoli ya Brazil kwa nguvu zetu zote. Tuache kuendeshwa na hisia bali tuendeshwe na fikra, kwani ujio wa timu ya Brazil hauwiani na msemo wa ‘mgeni njoo wenyeji tupone’, bali ni ‘mgeni njoo wenyeji tuzidi kuumia’. Mimi ninawatakia kila la kheri Brazil kwenye kombe la dunia na sisi kama kawaida yetu tutaishia kulishangalia kwenye runinga, kama utamaduni wetu, kwani sisi ni nambali moja kwa kushangalia maendeleo ya wengine na kuiga mambo yasiyo na manufaa.

Picha kwa hisani ya cartoonist Gado

4 comments:

  1. Hivi mbona mpaka leo hatujaambiwa hela zilitoka wapi? Kama ni wadhamini au watu binafsi, si wangetuambia tu ili tujue moja. Sasa hivi nasubiri taarifa ya hela iliyopatikana.. na watuambie zitatumika vipi (kama kuna faida yoyote ile.. maana'ke uwanja ulikuwa mtupu, wabongo wengi walalahoi. Wangapi wangeweza kuacha robo ya mishahara yao pale?).

    Ingawa napenda sana mpira, binafsi, ukosefu wa madawati mashuleni unanigusa zaidi! Kweli, mbona hizi juhudi za kutangaza nchi, soka na upuuzi mwingine zinazuka sasa hivi tu? Endeleeni basi hata kombe la dunia likiisha.

    TFF wanaweza wakasema hiyo sio kazi yao. Je, kutangaza utalii ni kazi yao? Mbona wanachagua kutumikia nchi pale tu wanapotaka (kwa manufaa yao)?

    ReplyDelete
  2. Hizo hela $2m/$3m/$6m ( not sure how much ) zingeweza kusaidia katika ligi za sekondari na shule za msingi. Maximo anaonekana anaelewa tatizo na ana vision. Kwahiyo angeweza kusaidia.

    Safari bado ndefu!

    ReplyDelete
  3. Nimepata habari kutoka BBC; inaonekana kama TFF watakula hasara:

    http://news.bbc.co.uk/sport2/hi/football/world_cup_2010/8728004.stm

    Nadhani itasaidia kupeleka maswali yetu kwa wahusika.

    ReplyDelete
  4. Yaani Bahati, everything you said here is so so true. Nimeshtuka kuona kua TFF haijatangaza wamewalipa Brazil kiasi gani truthfully... all this time I thought it was a friendly match meaning Tanzania haijacontribute zaidi ya kutoa labda accomodation and food for the Brazil players kumbe TFF wamewalipa mamilioni? aisee, kweli sometimes i wonder what people thing... na what their priorities are. wananishangaza kweli kweli.

    ReplyDelete