Nafahamu fika kuwa Vijana wengi hatupendi kufuatilia Siasa, hatuna mpango wa kupiga kura na hatufanyi mambo muhimu yanayohusiana na upatikanaji wa viongozi kwenye nchi zetu. Lakini, unadhani tutapata suluhisho la haya matatizo yetu kwa kunung'unika tu? Kupiga kelele kwenye forums?
Leo sina mengi sana kuhusu hili jambo, lakini napenda kuwaasa tufumbue macho na tujaribu kubadili fikra zetu. Tuitikie mwito pale jamii inapotuhitaji -- kuna matatizo mengi kila kona kama mnavyojua na ni jukumu letu kujitosa na kujaribu kuyatatua.
Nakusihi ufuatilie makala za Jenerali ulimwengu ambazo zinazungumzia uchaguzi ujao -- kuna mengi sana ya kujifunza.
Maneno ya Jenerali:
KATIKA makala zangu zilizopita nimekuwa nikijadili masuala yanayohusiana na uchaguzi mkuu ujao na jinsi tunavyojiandaa kukabiliana nao. Miongoni mwa mambo mengi ambayo nimejaribu kuyajadili nimekuwa nikisema kwamba sisi Waafrika bado hatujejenga uelewa wa kutosha wa kujua ni nini maana ya uchaguzi.
Bado tunaenenda, hasa tukiwa madarakani au tukiwashabikia walio madarakani, kama vile uchaguzi ni kitu kibaya ambacho hata hivyo hatuna budi kukivumilia kwa sababu, kutokana na sababu zisizozuilika, hakiepukiki. Hii ni sawa na kung’oa jino lililooza.
Ndivyo ilivyo katika nchi zote za Kiafrika. Uchaguzi ni jambo tunalokubali kuliingia shingo upande kwa sababu hivi sasa, katika dunia ya leo, hatutaeleweka duniani kote, na hasa kwa “wafadhili” ambao wanatuambia hatuna budi kuonyesha kwamba tunajali misingi fulani ya demokrasia.
Kama Waafrika, tunachoogopa hasa ni hatari ya kukosa misaada iwapo tutaonekana kama hatutaki kufanya uchaguzi. Tutanyimwa misaada, na kisha tutazomewa kila tuendako Ulimwenguni. Tutaonekana kuwa watu wa ovyo, watu wa zamani mno, watu wasio ‘poa.’
Kama isingekuwa mambo hayo mawili, naamini kwamba watawala wetu wangekuwa wamekwisha kutafuta lugha laini ya kutueleza kwamba uchaguzi ni jambo la hatari lililoletwa na wageni kwa lengo la kutuzuga na kutudumaza kwa kutufanya tuzame katika malumbano yasiyoisha ya kisiasa na tusahau mambo muhimu yanayohusu maendeleo yetu… kama kilimo.
Labda, wangeweza kuogopa kwamba wanasiasa wenzao katika upinzani wasingeikubali lugha hiyo na mantiki hiyo na wangeziingiza nchi katika migomo isiyoisha na ingewezekana hata kukatokea maasi kutokana na wananchi kuchoshwa na kundi linalong’ang’nia kuwa madarakani kwa kutumia kila hila ingawa ni dhahiri kwamba limeshindwa kufanya kazi ya kuwaletea maisha bora wananchi wao.
No comments:
Post a Comment