Miaka minne iliyopita nilikuwa sifuatilii vitu gani hasa vinavyotokea nyumbani, lakini nimekua na nimeanza kusoma vitu ambavyo vinanifungua macho. Na leo nimepata fursa ya kuperuzi bajeti yetu... Bahati mbaya bajeti yetu nd'o hivyo tena (bofya kwenye taswira):
Sio kama nimeshtuka saaaaana, ila kuna mambo mengi yanayoendelea ambayo yanatibua siku kama ya leo. Kama hicho kidogo tulichonacho, misaada na mikopo nchi yetu inayopata ingekuwa inatumiwa ipasavyo, sidhani kama ningekosa raha kiasi hiki.
Ni aibu kuendelea kuwapa madaraka watu ambao "labda" wanafanya mambo kwa manufaa yao. Tufanye nini? Ni kuwaondoa tu kwa nguvu ya hoja; nadhani kwa uchaguzi huu labda tume'shachelewa, kwahiyo tuanze kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa 2015? Ningependa kusikia mawazo yenu.
Nitaishia hapa na kuwaacha na maneno ya Jenerali Ulimwengu: Wawakilishi kama wafadhili, kosa!
Homa ya uchaguzi imepamba moto na wote wanaohusika kwa njia moja au nyingine wanachakarika. Wale wanaotarajia kujitokeza kama wagombea tayari wanapita huku na huku wakijitambulisha, na baadhi yao tayari wametangaza nia yao.
Miongoni mwa waliotangaza ni wale wale waliokuwa wabunge katika kipindi kinachomalizika hivi sasa, ambao wanatarajiwa wagombee tena, kwa sababu ni Waafrika wachache wanaokubali kujiuzulu kutoka katika nafasi za ‘uongozi’ ambazo mara nyingi ni nafasi za ulaji, ukwasi na utukufu. Nimesikia mara kwa mara watu wakishauri kwamba wabunge wasiruhusiwe kukaa bungeni kwa zaidi ya mihula miwili, lakini siamini kwamba siku moja Bunge letu litakuwa na busara ya kukubali ushauri kama huo.
* * *
... maana hii ya ubunge imevurugwa kabisa. Mbunge wa siku hizi anaangaliwa kama mfadhili, kama mtu wa “kuwaletea maendeleo” wananchi waliomchagua. Hiyo ndiyo lugha inayotumika: “Mkinichagua nitawaletea maendeleo.”
Dhana hii ambayo inamfanya mbunge kuonekana kama ‘mfadhili’ itatuumiza kwa muda mrefu, kwa sababu sioni ishara za kweli za kuifuta. Imekuwa ni njia moja rahisi kwa watu wasio na sifa za uwakilishi kujipatia ajira, nao wataiendeleza dhana hiyo kwa sababu inawafaa. Wananchi wenye sifa na uwezo mkubwa wa kuwa wawakilishi hawatafua dafu kwa sababu hawana uwezo wa ‘ufadhili’ huo.
* * *
Kwanza kabisa, wananchi waelimishwe kuhusu maana halisi ya mbunge kama mwakilishi, kama mjumbe, na siyo kama mfadhili, na dhana hii ieleweke vyema kwa wananchi. Wanaposhiriki katika michakato ya uchaguzi wajue kwamba hao wanaowachagua si watu wa “kuwaletea maendeleo” kama wanavyowaangalia “wafadhili” bali ni wajumbe wao ambao jukumu lao kuu ni kuwawasilishia matatizo yao na hoja zao katika baraza la Taifa na huko ndiko upatikane ufumbuzi wa matatizo yao katika muktadha wa kutafuta utatizo wa matatizo ya nchi nzima kwa pamoja.
Tusiwaruhusu wabunge wetu kujifanya ni Papa Noeli, Father Christmas anayekuja na zawadi kwa kila mtoto, kwa sababu mbili kuu: kwanza katika dunia ya kweli hakuna Father Christmas; pili tunatakiwa tuache kuwa watoto.
No comments:
Post a Comment