Tuesday, June 1, 2010

Waafrika tuna asili moja?

Na VR

Kwa muda mrefu nimekuwa nikiumia roho mno kwa jinsi watu kutoka Afrika tunavyolundikwa kwenye kundi moja kiasilia. Kukiwa na tatizo utasikia, waache hao, ni tabia ya Waafrika hio, hawatakoma. Bara/nchi yao imelaaniwa.

Ukweli ni kwamba bara letu lina watu wenye asili na tofauti nyingi mno kimaumbile, kiutamaduni na hata ukiingia kwenye chembe chembe za DNA. Ukiangalia bara la Ulaya, Wajerumani wamepakana na Wafaransa, lakini watu hawa hawapendi kabisa kufananishwa. Ukienda Amerika ya Kusini, ni mwiko kumuita mtu anayetoka Colombia Mbrazili.

Utafiti unaonesha kwamba idadi kubwa ya watu wenye asili ya Afrika wana maumbile mengi na tofauti kuliko watu katika mabara mengine -- hasa ukiangalia chembe chembe L1, L2 na L3 mtDNA (Krings et al, 1999).

Wanahistoria waliojaribu kutafuta jinsi ya kuelezea asili ya Mwafrika, walifanikiwa kusambaza mawazo yao pande zote za dunia. Mengi ya mawazo hayo yawezekana yalikuwa ya kudhani tu au imani. Inasemekana kuwa asili ya Mbantu ni misitu ya Kongo. Ingawa yawezekana ikawa ni kweli, nina hofu ikawa ni imani ya wenyeji wa pale waliodhani kuwa wako katikati ya dunia. Na mtafiti aliyefika pale hakuweza kupata mawazo ya staarabu, makundi au falme nyingine zilizokuwa mbali na eneo utafiti huo ulipofanyika.

Kwahiyo elimu iliyopatikana hapo haikuwa ya kutosha au tuseme ilikuwa hafifu. Ingawa mtafiti huyo alilifahamu hilo, aliamua kufanya hitimisho kuwa Wabantu wote walitokea eneo lile. Ninaweza nikahisi kuwa, Kibantu asili kama ilivyokuwa Kilatini na sasa Kiingereza, ilikuwa lugha ya wasomi wa kale hapa Afrika. Sasa, idadi ya watu wenye asili tofauti ilivyokuwa inaongezeka, lugha nayo ilikua na kubadilika taratibu ingawa iliendelea kuwa na asili yake miaka nenda rudi. Hitimisho hili halina uhakiki kuwa asili ya Wabantu na hasa watu wa kusini mwa jangwa la Sahara wawe na asili ya misitu ya Kongo. Cha kushangaza, chembe L0 mtDNA inayosemekana kuwa mzazi wa L1, L2 na L3 mtDNA, inahisiwa kuwa na chanzo chake Afrika Mashariki.

Kwanini Waafrika tukubali kuwekwa kwenye kundi moja kiasilia? Je, uanzishwaji wa Umoja wa Afrika unaangalia tofauti kubwa zilizopo za utamaduni na asili kati ya makundi mbalimbali hapa Afrika kwa nia ya kuboresha sera za muungano huo? Makala hii itaendelea na uchambuzi wa kina zaidi kuhusu hili jambo.


Picha/ramani inapatikana hapa.

2 comments:

  1. Kwanza, asante...

    Lakini kabla ya kuchangia ningependa kusema haya au kuuliza maswali yafuatayo (nadhani makala nyingine kuhusu hili suala zitafuata).

    Umeanza kwa kuongelea mambo mawili; asili ("nature"?) na tabia za watu (ambayo inaangukia upande wa mambo ya kijamii zaidi -- social aspects of life; sina uhakika kama tunaweza kutumia "nurture" kwenye mfano uliotoa..).

    Binadamu tuna tabia ya udadisi (naamini) ndio maana hela nyingi zinapelekwa kwenye tafiti kama hizi. Lakini, huoni ni hatari kuzungumzia asili na tabia za kundi au jamii fulani kwa kutumia biology tu? Ndio, vitu kama nywele, midomo na maumbile kwa ujumla vinaweza kuelezwa kwa kutumia biology. Lakini, ulipozungumzia ile "generalization", ulimaanisha ni maumbile/asili na/au tabia?

    Kwasababu sidhani kama tunaweza kuelezea kila kitu kwa kutumia nadharia moja tu -- tunakuwa too deterministic; ningependa kusikia nadharia za social psychologists, anthropologists na wengineo hasa linapokuja suala la tamaduni/tabia/desturi.

    Nawasilisha.

    ReplyDelete
  2. Nice article. We need this variety in the TZ blogosphere scene.

    ReplyDelete