Wednesday, June 16, 2010

TAMASHA-Vijana na Ujamaa Hip Hop Darasa

Ukiperuzi haraka haraka kwenye hii makala unaweza ukadhani umepotea njia na uko kwenye blog ya Fid Q. Hapana -- hapa ni Vijana FM, mzee!

Kama nilivyosema wiki chache zilizopita, kuna baadhi ya mambo au harakati zinazofanywa na Vijana wenzetu ambazo mara nyingi hazitambuliwi; kwa maneno mengine, inaonekana hazipewi kipaumbele. Lakini nadhani Vijana FM itabadili hii desturi.

Nia hasa sio tu kuwafagilia tu Vijana wenzetu. Ni matumaini yangu kuwa makala kama hizi zitawapa wahusika changamoto na kuwahamasisha Vijana wengine kujiunga na kuwasaidia wahusika kwa namna moja au nyingine.

Leo hii nakuletea harakati za Winston Churchill na timu yake nzima ya TAMASHA-Vijana. Mchana wa leo (tarehe 16 Juni, 2010) ulikuwa ni maalumu kwa ajili ya Watoto wa Afrika, na mzee mzima Fid Q ndio alikuwa mgeni rasmi au mwalimu wa kwanza wa Ujamaa Hip Hop Darasa.

Kabla sijakupa dondoo za hili Darasa, ningependa kukuambia madhumuni hasa ya TAMASHA-Vijana/Ujamaa Hip Hop Darasa.

Winston anasema,"[Tunajitahidi] kufikiria jinsi ya kuwasaidia Vijana... maana tunaona wana vipaji lakini jinsi ya kuvibadili katika ujasiriamali bado imekuwa ndio changamoto. "

Kwahiyo wameamua kuanzisha Ujamaa Hip Hop Darasa. Hili Darasa litakuwa linatumia falsafa ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere: "Binadamu hujikomboa na kujiendeleza mwenyewe; hawezi kukombolewa na kuendelezwa." Na litakuwa linatumia taswira ya utamaduni wa Ujamaa wa Kiafrika na Hip Hop ili kuwavutia zaidi Vijana.

Darasa rasmi la kwanza la Hip Hop litaanza tarehe 26 Juni (Mikocheni, Old Bagamoyo Rd, Dar es Salaam). Licha ya kwamba Madarasa yatakuwa bure, waandaji bado wanafikiria namna ya kufanya mpangilio mzima uweze kujiendesha wenyewe.

Ukiacha Hip Hop Darasa kuna mambo mengine yatakayokuwa yanaendelea na kufanyiwa kazi -- kwa mfano, utengenezaji wa video (Research, Archive and Documentary on Hip Hop), Outreach and Relations, Uhuru Clothing na Film Project.

Napenda kuchukua fursa hii kuwatakia kila la kheri TAMASHA-Vijana na Ujamaa Hip Hop Darasa kwenye shughuli zao na nadhani timu ya Vijana FM itajaribu kuwasaidia pale itakapoweza.

Cha muhimu zaidi ni wasanii wengine, wataalamu wa mambo haya na Vijana kwa ujumla kuitikia mwito.

Nawatakia jioni njema!

1 comment: