Monday, May 24, 2010

Watanzania Tunaogopa Sayansi? Sehemu ya Pili


Particles
. Mlipuko. Mlundiko wa data. Haya ndio yatokanayo kwenye matembezi niliyofanya na wenzangu kwenye saiti ya tafiti ghali kuliko zote duniani: saiti ya Large Hadron Collider pale CERN. Ndani ya bomba la duara lenye uzingo wa kilomita 30 hivi, protoni zinakimbizwa kwa spidi ya kilomita 299000 kwa sekunde ili kusababisha mlipuko mdogo pindi zinapogongana. Mlipuko huu unatumiwa kufahamu sifa za vihimili viundavyo maada (matter), pamoja na siri mbalimbali kuhusu ulimwengu wetu.


Katika safari hii sikujisikia mpweke. Nasema hivi kwani sikuwa pekee ambaye hakuwa na kisomo cha juu cha fizikia. Kulikuwa na watu kama hamsini niliowaona, wa kila rika, wakipishana katika korido za saiti. Nyuzi iliyowaunganisha ni nia ya kufahamu kiujumla kuhusu sayansi ifanywayo nchini mwao. Ni fikra kama hizi ambazo ningependa kuhimizwa nyumbani kwetu. Je, saiti ya Apopo inapokea wageni wazawa wangapi? Makumbusho ya taifa je? Tume ya sayansi (COSTECH) je?

Bajeti ya utafiti wa CERN ni T.Shs Trilioni 1 kila mwaka. Wengi wetu tunaweza kushikwa na hisia na kuwakasirikia na kuuliza kwanini wanatumia pesa nyingi hivi kwa tafiti kama hizi zisizokuwa na uhakika? Wakati huohuo mamilioni ya watu wanakufa kwa ukimwi, malaria na njaa kila mwaka. Binafsi ninadhani mpaka tutakapofahamu umuhimu wa sayansi kwa manufaa yetu wenyewe (waTanzania), hatuna haki ya kuwa na hisia hizi. Sayansi yetu ya kupambana na haya majanga inahimizwaje? Au jamii yetu tutabaki kushabikia akina dokta manyau tu.

Spidi ya hatua zilizopigwa na wenzetu kwenye sayansi inastaajabisha. Na kutambaa kwetu katika lengo hili hili halitazaa matunda kama hatutaamka. Tunahitaji kufinywa na kuhimiza sayansi nyumbani.

6 comments:

  1. tunahitaji kweli hiyo sayansi?

    ReplyDelete
  2. Shukrani kwa kutupa mwangaza.

    Kitu ambacho kinanifurahisha na ningependa labda na jamii yetu ijifunze ni kujishughulisha na kutaka kujua nini kinachoendelea kwenye sehemu kama hizi. Nadhani maabara kama hizi zina open days ambapo kila mtu anayetaka kujifunza au kuona tu kinachoendelea anakaribishwa.

    Unaweza ukadhani ni kitu kidogo tu. Lakini ukweli ni kwamba ziara kama hizi ndizo zinazowapa motisha wanafunzi wa miaka ya baadae. Na walipa kodi nao wanapata kuona nini kinachoendelea; kuulizia wapi hela zao zinapokwenda.

    Mara nyingi, kutokana na watu kutoelewa undani wa experiments zinazoendelea watu wengi hupotoshwa na vyombo vya habari. Kwa mfano, mwaka 2008 wakati huu mradi unaanza watu walidhani utakuwa ndio mwisho wa dunia kwasababu kulikuwa na uwezekano wa black holes kutokea. Lakini kama watu wangekuwa wanawasikiliza wataalamu wenyewe, nadhani hofu isingekuwa kubwa (wanajua ni nishati kiasi gani 'wanayocheza' nayo).

    Sasa, huu mradi hatujui matokeo yake. Lakini kama ukifanikiwa kuna uwezekano mkubwa sana ya kwamba utatufumbua macho -- na kuwasukuma watu kufanya tafiti za nuclear energy zaidi!

    Kuna mradi mwingine mkubwa sana wa nchi za EU (ITER) uko mbioni (kwa ajili ya fusion energy):

    http://www.iter.org/default.aspx

    Pia, napenda kuwaasa hata wale ambao hawajabobea kwenye sayansi kusoma makala ndogo ndogo kuhusu haya mambo.

    Kusema ukweli natamani nilivyokuwa mdogo ningeona sehemu kama hizi. Labda ningeishia kwengine kabisa.

    ReplyDelete
  3. Sikuliona swali la mchangiaji wa kwanza.

    Kwa mtazamo wangu - mimi binafsi - nadhani TUNAHITAJI sayansi. Angalia nchi zinazoendelea jinsi wanavyowekeza kwenye tafiti. Ujue mpaka leo kuna matatizo kwenye jamii yetu ambayo yangeweza kutatuliwa kwa tafiti za kisayansi - njia za vilimo, kujikinga na magonjwa (ya tropiki) n.k.

    Kama unazungumzia mradi huu pekee, basi huu utakuwa mjadala mwingine. Kama unataka kuelewa soma makala ifuatayo:

    http://vijanafm.blogspot.com/2010/04/watanzania-tunaogopa-sayansi.html

    ReplyDelete
  4. Madogo wanaosoma sekondari ktk masomo ya sayansi option zao ni: ukisoma PCB lazima ukasome Medicine, ukisoma PCM/PGM wengi macho yao ni Uhandisi kama first choice. Career in science hazijulikani kwa wengi, role models hawapo au kama wapo ni wachache mno.

    ReplyDelete
  5. sayansi bongo?!

    ReplyDelete
  6. ...Tatizo kubwa la nchi yetu ni kwamba uhamasishaji wa elimu upo kwenye nadharia badala ya vitendo...vile vile napenda kusema kuwa lugha itumiwayo kwenye shule nyingi za umma ni kiswahili...hili tu ni kikwazo kikubwa mno ukizingatia kuwa ngazi yetu kisayansi iko chini sana. Nasema hivi kwa kuwa, makala nyingi na vitabu huchapishwa kwa kiingereza, hata wajerumani na waspanyiola wameamua kuwasilisha uvumbuzi wao kisayansi kwa kutumia kiingereza. Kwa ujumla, kama kilatini kilivoyokuwa lugha ya wasomi zama za kale, kiingereza ni lugha ya wasomi wa zama za sasa. Kwahio, ni vigumu kwa wanafunzi/watoto wetu kujieleza kisayansi au kuelewa sayansi isiyokuwa na visawe au maneno wakilishi kwa lugha ya kiswahili. Sisemi kwamba kiswahili hakifai, la, namaanisha kuwa pamoja na kwamba twahitaji lugha yetu - urithi wetu ukue, ni muhimu sana kwenda na wakati ilhali tunakipigania maendeleo ya kiswahili. Kwa ujumla mitaala ya elimu ya kitanzania kuanzia shule ya awali mpaka chuo kikuu, inabidi iangaliwe upya na mawazo ya kimapinduzi yafikiriwe kulingana na mazingira yetu, yaongezwe na kutumiwa kwa faida ya vizazi vijavyo.

    ReplyDelete