Sunday, April 4, 2010

Harufu ya Kifua Kikuu (TB)

Kilimota kama 5 hivi kutoka Morogoro mjini, pembezoni mwa mlima Uluguru, kuna shule moja maalumu yenye wanafunzi wenye vipaji. Wanafunzi hao, viumbe ambao jamii tunawachukia kwa udi na vumba, wanapata elimu ambayo yaweza kusaidia katika mapambano ya ugonjwa wa kifua kikuu (TB). Viumbe gani hawa? Ni panya buku. Wanasayansi wa chuo cha Sokoine na wenzao wa Ubelgiji wameanzisha utafiti wa kuwatumia panya ili wawe na uwezo wa kuaguza (to diagnose) TB.


Nchi yetu ni moja ya nchi zilizoathirika kwa kiasi kikubwa na ugonjwa wa TB. Hali hii imezidishwa hasa kutokana na tatizo la Ukimwi tunalopambana nalo, kwani wagonjwa wengi wa Ukimwi wanakuwa pia na TB. Uaguzi wa mapema wa TB ni muhimu ili kuweza kudhibiti ugonjwa kabla haujawa sugu. Kwahiyo, changamoto iliyopo ili kupunguza vifo na taabu ya ugonjwa huu ni kuutambua mapema mno.

Njia mbalimbali zinatumika sasa kuaguza TB, mfano vipimo vya kukuza vinasaba (PCR), X-ray, kupima ukohozi kwa microscopy, vipimo vya ngozi n.k. Tatizo ni kwamba, vipimo hivi ni ghali na upatikanaji wake ni wa shida katika hospitali na zahanati zilizopo vijijini, sehemu zenye waathirika wengi. Jambo lingine ni kwamba, utumiaji wa microscopy, njia ambayo inatumika kwa wingi Afrika haina usahihi wa hali ya juu (kati ya 20-40%).

Tukirudi Morogoro, watafiti wamejaribu kutumia uwezo wa panya buku kunusa harufu adimu na kuutumia katika kugundua TB. Yasemekana kuwa, bakteria wanaosababisha TB, Mycobacterium tuberculosis, wanatoa harufu ya kemikali fulani (volatile organic compounds) ambazo zina pattern fulani. Wanachofanya ni kuwapa sample ya kohozi kutoka kwa muathirika na kumfundisha panya kugundua kwa uimara harufu hizo. Uwezo wa panya hawa kugundua TB ni mkubwa (zaidi ya 85% specificity na sensitivity) na cha kufurahisha ni kwamba, panya buku wanaweza kufundishwa kukumbuka hizi harufu. Mradi huu, ulioitwa APOPO ni wa kipekee kwani unatumia rasilimali tulizonazo ili kukabiliana na matatizo yetu.Ni changamoto kwa vijana wetu kuweza kutumia njia mbadala katika kupambana na matatizo yanayotukabili. Wanafunzi wa umeme na kompyuta wanaweza sasa kushirikiana na hawa wa Apopo ili kuweza kutengeneza vifaa portable ambavyo vitatumika hospitalini. Hii ni katika kuendeleza tafiti.

3 comments:

 1. Fascinating, hakika hii ni hatua muhimu.

  ReplyDelete
 2. hii poa sana, nadhani huu ufumbuzi ni kitu ambacho tanzania tunaweza kujivunia. Pia, ninakubaliana na swala la wanasayansi wa kitanzania kuungana na huu mpango, hata kuangalia ni jinsi gani tunaweza kutumia asilimali tulizonazo kutusaidia kuliko kusubiri vitu kutoka nje.

  Hawa jamaa nimewakubali, nadhani sirikali inabidi itazame mipango kama hii na hapo hapo kusukuma wanasayansi wa kitanzania na kazi zao, na kutengeneza mfumo wa kuchochea ubunifu na maendeleo katika sayansi na tafiti zake kwani kufanikiwa kwa sayansi, ni kufanikiwa katika maendeleo ya nchi.

  ReplyDelete
 3. Inatia moyo kusikia mambo kama haya na nadhani labda itasaidia kuwapa motisha watu, hasa vijana ambao inabidi wajifunze kuwa wadadisi.

  ReplyDelete