Saturday, April 24, 2010

Viumbe hai nje ya sayari yetu

Msomaji, nina uhakika unajua tarehe yako ya kuzaliwa. Lakini sijui kama unakumbuka mambo yaliyokuwa yanajiri wakati mama yako anajifungua. Kumbukumbu zote ulizonazo kuanzia sekunde ulipoanza kupumua mwenyewe hadi kipindi unaanza kutambaa zimetokana na picha au hadithi na simulizi ulizosikia kutoka kwa wazazi, ndugu na marafiki wa karibu na familia yako.

Je, kuna wakati unakaa chini na kutafakari mwanzo wako ulikuwaje? Nini kilikuwa kinatokea kwenye maisha yako kabla hujaanza kuota meno?

(Chanzo)

Uelewaji wako wa mazingara na mazingira yanayokuzunguka unazidi kupanuka kadri unavyokua; lakini labda wewe ni mmoja wa wale ambao hutafakari kwa kina na kujaribu kubadilisha mawazo ya awali (wakati bado uko mdogo) ili kutengeneza picha inayokaa vizuri kwenye akili yako. Na kama hii haitoshi, unaanza kurandaranda na kucheza na vitu mbalimbali - vingine ni hatari - ili tu kukidhi ile haja ya kujua vitu.

Au kama una bahati, ulikuwa na watu ambao walikuwa wako tayari kukuelezea mambo mbalimbali yaliyokuwa yanakutatiza. Na kama ulikuwa una bahati sana, ulizungukwa na watu ambao walikuwa wako tayari kukupa hata vifaa vilivyokusaidia kuona na kuelewa vitu gani hasa vipo karibu na sayari yetu.

Binadamu tuna tabia ya udadisi -- tunataka kujua na kuelewa vitu vingi. Tunaweza kumlaumu Hanno The Navigator (huyu alianza 'kuzurura' kwenye miaka ya 500 Kabla ya Kristo!). Au tuwalaumu Wareno?


Ruka karne 4...

Kizazi chetu kimekuwa na bahati ya kushuhudia mapinduzi katika teknolojia ambayo hutusaidia kujifunza mambo mbalimbali na kuturahisishia maisha kwa ujumla. Bahati mbaya teknolojia hiyo hiyo imekuwa inatuletea zahma mara nyingine (soma kuhusu Manhattan Project 1942-46; huu ni mjadala wa siku nyingine)!

Ukitafakari kwa makini utaona kuwa tabia za watoto wadogo na sayari yetu zinarandana. Wakati uko mdogo unakuwa kwenye fikra zako ambazo hakuna kiumbe mwingine anazielewa na unadhani uko peke yako. Lakini kadri unavyozidi kukua ule mtazamo unabadilika -- watu walio karibu nawe hukusaidia kuelewa yanayokuzunguka.

Kwa upande mwingine, sayari yetu tulidhani ni pekee. Lakini sasa hivi tunajua kuwa kuna vitu vingine ukiacha hii dunia. Teknolojia (ambayo unaweza kuilinganisha na watu wanaomzunguka mtoto mdogo) imetusaidia kujifunza nini hasa kilichopo karibu na hii sayari yetu.

Kuna wanasayansi ambao wanajaribu kutafuta viumbe hai nje ya sayari yetu. Na hawaishii hapo tu; wanaamini wameanza kuona dalili za uwepo wa viumbe vyenye akili. Hapa nazungumzia intelligence -- uwezo wa kufikiria, kutatua matatizo, kuwasiliana, kujifunza vitu vipya n.k.

Kwenye filamu fupi ifuatayo Jill Tarter anaongelea programu ya SETI na utafiti wao wa kutafuta civilizations nje ya sayari yetu:Unadhani tuko wenyewe kwenye ulimwengu mzima? Au unaamini watu wa SETI watafanikiwa? Je, teknojia yetu inatupumbaza tu na kutupa 'kiburi'?

Kwa kuwa hakuna faida yoyote, hizi hela si zingetumiwa kutatua matatizo ya nishati kwenye sayari yetu?...Napenda kusikia mawazo yenu!

3 comments:

 1. Nadhani tafiti hizi zina umuhimu wake. Ila, I think it is a great challenge to receive a signal from another civilization in the universe. As in the probability of finding a civilization with apt technology that create signals that we can detect at this particular point of time is really limited. Nina uhakika SETI wanalijua hilo, ila hili ndio dukuduku langu. I just think the search for any sort of life elsewhere in the universe is more exciting to me (be it virus, bacteria or plant-like), let a lone the search for intelligent life.

  ReplyDelete
 2. http://edition.cnn.com/2010/OPINION/04/27/tarter.space.life.fears/index.html?hpt=C2

  http://www.youtube.com/watch?v=L2oYS9-Ee9U

  ReplyDelete
 3. Joji, shukrani kwa hizo links...Nilikuwa naitafuta hiyo documentary.

  ReplyDelete