Friday, April 23, 2010
Barua: Samahani Wanangu
Yah: Shukrani kwa Mh. Mrisho
Mheshimiwa Mrisho nashukuru sana kupata ujumbe wako wa msamaha, umefika na nimeukubali, kwani moyo sio jiwe hivyo yaliyopita si ndwele bali tugange yajayo. Moyo wangu umeshikwa na faraja kubwa sana kujua leo hii wizara yetu husika imepata kiongozi anayetufahamu fika sisi vijana na shida zinazotukabili. Mimi ni kijana wa Kitanzania niliyejawa na vidonda vya shida, uso weyenye simanzi na hofu iliyonitanda kama upele mwilini. Miaka mingi sasa sauti yangu imelazimishwa kujifungia ndani na kuishi kama mkiwa, kwani jamii haitaki kuisikia kwani mimi bado ni taifa la kesho. Hivyo, dukuduku langu ndani lilikuwa limeanza kuwa sumu, lakini nashukuru umekuja ukaniokoa kwa kumulikia sauti yangu iliyotengwa na viongozi na jamii kwa miaka mingi.
Barua yako imeanza kunipa matumaini na Serikali yetu kuwa kweli ina nia ya dhati katika kujali nafasi yetu sisi vijana ndani ya jamii. Matumaini yangu ni kuwa busara zako zitawafikia wazee wengine na wataanza kutuona, hivyo na wao kuanza kututhamini na kutusaidia kwa hali na mali. Hapa kijijini wazee wamekalia ardhi yote, na huko mjini nasikia vijana wanafukuzwa eti warudi kijijini kuja kulima. Mh waziri Mrisho, najua kizazi chetu ni kama kilicholaaniwa, wezi ni sisi, machangudoa wanaosimama mabarabarani ni sisi, wakataa kwenda shule za matope na nyasi ni sisi, lakini nani mchangiaji mkubwa wa yote haya? Hilo halipunguzi furaha yangu juu ya barua yako inayoonyesha kujali utu wetu kama wananchi wa nchi hii na sio kama wageni kutoka sayari nyingine.
Ningependa kumalizia kwa kukuhakishia kuwa, tunapoongea juu ya matatizo yetu nia sio kuwakosea heshima wakubwa zetu. Sisi hatuna makuu bali tunaomba kusikika, kuthaminiwa, kwani mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Barua yako imenipa tabasamu lililopangusa pangusa vumbi lililokuwa limejaa juu ya paji la moyo wangu. Naomba nisalimie waheshimiwa wengine , ukiweza wapatie barua yangu wasome. Waheshimiwa wakikuuliza kwanini sikuandika kwa Kiingereza, naomba uwajulishe kuwa mwalimu wa Kiingereza tuliyehaidiwa hakuwahi kuja kufika. Pia, sikutaka kuifanya hii barua iwe katika mandhari ya kibongoflava music, kwani najua waheshimiwa wanadhani ni mziki wa kihuni, bila kujua sanaa hiyo imepatia ajira vijana wengi na kutupa vijana sauti yetu inayo nyanyapaliwa kwa kawaida na jamii. Asante tena Mh. Mrisho na utaniwia radhi kwa kukuita waziri kwani baada ya kupata barua yako nilidhani wewe ndio waziri wa wizara yetu sisi walengwa. Asante sana na ninakutakia mema mbeleni, na ninakuomba usisahau kutukumbuka tena sisi vijana.
Wako kijana wa Tanzania,
anayejitahidi vilivyo kuendelea kuwa raia mwema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment