Friday, April 16, 2010

Unapenda Mpira kuliko Elimu?

Jezi za timu zetu zilikuwa hazina majina ya wachezaji migongoni (na tunajua kwanini ilikuwa mwiko kwa wachezaji kubadilishana jezi baada ya mechi!). Lakini kila mtu - hasa mabeki wa vilabu Afrika Mashariki nzima - walikuwa wanajua kuandika "Edibily Jonas Lunyamila" kwa ufasaha. Ndio, jina la yule winga machachari aliyekuwa anatumia guu la m@#i! Hakika alitingisha Afrika Mashariki alipokuwa anavaa uzi wa njano.
Wengi tulikuwa tuna ndoto za kuwa kama Lunyamila, Mohammed Hussein "Mmachinga", Thomas Kipese "Uncle Tom", Kizota, Gagarhino...Nilishawahi kuota nawapiga 'matobo' mabeki kama Lunya; kupiga mashuti kama Chinga; kuteleza kwenye chaki kama Kipese; kupewa kadi nyekundu baada ya kupiga mabeki 'vipepsi' kama Kizota; na kuchana nyavu kama Gagarhino (hivi ni kweli jamaa alichana nyavu alipopiga penati dhidi ya timu ya Sigara?)! Tafadhali usiniulize ndoto zangu zimefinifikisha wapi - maana'ke itanibidi niandike kitabu ili kujibu hilo swali tu!

Kutokana na sababu mbalimbali baadhi ya wachezaji waliamua kusitisha masomo yao ya sekondari ili kujiingiza kwenye kabumbu ya ridhaa Tanzania. Sina uhakika, lakini kulikuwa na tetesi kuwa mmoja wa wachezaji maarufu aliingia kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga wakati yupo kidato cha tatu na kuamua kuachana na shule baada ya 'kuhitimu' kidato cha nne.

Ndoto za kizazi cha sasa zimebadilika. Sasa hivi Vijana wana ndoto za kucheza mpira wa kulipwa nje ya nchi, hasa Ulaya. Sipingi kuwa Bongo kuna vipaji vingi sana, lakini huwa nashtuka pale Kijana anapoamua kuweka vitabu pembeni ili kujaribu kutimiza ndoto zake. Kwa kifupi, vikwazo ni vingi sana kwenye safari ya kuwa mchezaji wa kulipwa. Ukiangalia safari za Vijana wengine kutoka nchi mbalimbali waliofanikiwa utakubaliana nami kuwa ni kama kamari. Kuna kujeruhiwa, suala la kupata timu inayokufaa na kocha ambaye atakufanya ujiamini, na muhimu zaidi kuliko vitu vingine vyote ni kuwa utahitaji bahati sana.

Siwezi kuweka wachezaji chipukizi wote kwenye kundi moja; lakini itakuwa ni jambo la busara sana kutokimbia umande hadi pale utakapokuwa na uhakika kuwa utafanikiwa kwenye mpira wa kulipwa.

Pia, mawakala, makocha na watu waliokuwa karibu na wachezaji wenye ndoto za kusakata kabumbu Ulaya hawana budi kuwapa picha halisi na mawaidha ya busara kama The Right to Dream Academy ya Ghana inavyofanya.



Tunajua wapi wachezaji wengi wa Tanzania walipoishia na wanapoishia. Lakini, unadhani labda mambo yangekuwa tofauti kidogo kama wangejaribu kujiendeleza na mambo mengine? Bila shaka wangekuwa na fani nyingine baada ya kumalizana na mpira - hasa ukizingatia mpira wa kulipwa ni kazi ya miaka kumi hadi kumi na tano tu.

4 comments:

  1. Hao watajwa hapo juu kuna mtu anafahamu wanajishughulisha na nini? Lunyamila, Mohammed Hussein "Mmachinga", Thomas Kipese "Uncle Tom", Kizota, Gagarhino.
    Je wanaendelea kusaidia kukuza soka la nchi?

    ReplyDelete
  2. Anon, Kizota alifariki baada ya kugongwa na daladala...

    ReplyDelete
  3. Oya SN ..nimeipenda hii atiko...nilikuwa nacheki hiyo picha sura zote zipo kichwani but majina yamitoka kidogo..but namuona kipa wetu mashuhuri Stephen Nemes (alikuwa noma kasoro kwenye penati...afu sijui alipata wapi jina lake la uko), namuona Ken Mkapa white katikati...namuona Sekilojo Chambua kule chaki...namuona kizota, namuona Mohamed Husein......Je unamkumbuka James Tungaraza...bolizozo (named after jamaa wa Stella Abidjani waliowafunga Simba fainali CAF?....Simba haikuwa timu yangu but looking back nadhani ile ilikuwa accomplishment kubwa ya klabu za TZ kulik ziote) . Unaongea ukweli mkubwa...mi nilivokuwa mdogo nilikuwa najua future yangu ilikuwa kwenye mpira (has nothing to do on whether i had what it takes or not)...nadhani pia wachezaji ndo walikuwa marole model flani ambao walikuwa wanajulikana collectively na watu wengi....Lakini unavozidi kuwa mkubwa unaona kuwa mpira siyo dili kiivyo baada ya kuona wachezaji wanavoishia au wanaoishi nk.

    Kuhusu elimu nadhani inabidi kuwa na mfumo ambao una-emphasize both elimu ya kawaida na michezo. Kuwa na shule za michezo ni muhimu kwa kukuza vipaji lakini hizo shule inabidi ziwe na conditions za mtu kusoma (na kufaulu--muhimu hii condition) masomo ya kawaida pia......watu wanaofanikiwa kwenda kwenye wanamichezo ya kulipwa (bongo au ulaya) ni asilimia ndogo sana ya watu wanao-aspire kuwa wanamihezo wa kulipwa kwa hiyo mwisho wa siku...kwenye darasa la watu 100 labda kumi tu ndo watakaofika na wengine inabidi wawe na nyenzo za kufanya vitu vingine maishani. Elimu pia inasaidia wale waendao waweze kuwa na upeo zaidi especially wakiwa wanataka kucheza nje ya nchi.......

    ReplyDelete
  4. "but namuona kipa wetu mashuhuri Stephen Nemes"..
    Nadhani mashabiki wa Simba wamesusia mjadala!

    Nawakumbuka wote uliowataja. Kuhusu takwimu ulizokisia, nadhani ni ndogo zaidi. Labda mmoja au wawili tu wanaofikia kiwango cha juu.

    ReplyDelete