Monday, April 12, 2010

Hatuna Kiongozi...

...pale maji yanapotufika shingoni Vijana wa Tanzania.
Kuna mambo ambayo hujiri na yataendelea kujiri kwenye jamii yetu kila kukicha. Baadhi ya mambo huhitaji hatua muhimu kuchukuliwa; kuanzia mijadala, mipangalio hadi maamuzi ya nini kifanyike kuweka mambo sawa kufuatana na matakwa ya wengi. Mengi sana yametokea nyumbani kwenye mlongo uliopita lakini inaonekana Vijana wengi tumesahau nini Shaaban Robert alichotuasa. (Kama ulikimbia umande, naongelea suala la viongozi na wananchi kujitoa mhanga lilojadiliwa kwa kina kwenye kitabu cha "Kusadikika".) Inaonekana wengi wetu tulisoma na kukariri sentensi kadhaa tu ili tusifeli mitihani ya Kiswahili.

Ukijaribu kujikumbusha mambo kadhaa yaliyotokea - hasa rushwa na ubadhirifu - utaona kuna kama mtiririko fulani unaotabirika: Tunaanza kwa kupiga kelele, kuendelea kupiga kelele, kupiga kelele zaidi, kuwalaumu viongozi wetu, halafu mwishowe 'tunasahau' kabisa. Sasa jaribu kujiweka kwenye nafasi ya madaraka halafu upenyo wa kujilundikia mali unajitokeza. Naamini fika kuwa wengi wetu tutaishia kuwa mafisadi! Hii hutokana na kutokuwa na mkwara tosha; mafisadi wengi wanajua Watanzania ni watu wenye hulka ya upole na tusiojua kupigania haki zetu.

Ukiangalia kwenye vyombo vyetu vya habari na kufuatilia mijadala inayoendelea kwenye forums na blogs mbalimbali utaona kuwa hatuna viongozi. Hakuna watu wanaoweza kuwasihi na kuwapa motisha watu kupigania haki zao (hata zile za msingi). Na cha kusikitisha zaidi hatujadili kabisa "nini kifanyike" na kubaki kutapatapa kwenye maji ya kina kirefu! Lakini kuna dalili kuwa Vijana wanaanza kuamka, ila kwa mwendo wa kinyonga.

Wengi bado wanaendelea kumlaumu Mwalimu na Siasa ya Ujamaa. Lakini, angalau alikuwa ana ndoto zake ambazo aliamua kuzipigania. Alijitoa mhanga na juhudi zake na uwezo wa kutuunganisha zimetufikisha hapa tulipo na kutupa misingi ya Taifa letu kwa ujumla. Hata kama hukubaliani na Siasa za Ujamaa na Kujitegemea, nitashaanga sana usipoafiki kuwa alikuwa ana hulka ya kiongozi - kuwakutanisha watu na kuwapanga ili kufikia lengo fulani. Natamani sana tungekuwa na watu kadhaa kama Mwalimu waliokuwa na mitazamo tofauti.

Angalia kushoto, kisha kulia, halafu niambie ni nani ambaye anapaswa kupewa heshima na kuangaliwa kama kiongozi wa Vijana. Bila shaka majina kama Kabwe na Slaa yatakuwa kwenye vinywa vya watu. Lakini sidhani kama kuna mtu ambaye tunaweza kumchukulia kama taswira ya Vijana wa Tanzania.

Binafsi naamini kuna watu ambao wanaweza kuwa viongozi na kutusaidia Vijana pale tunapokumbana na vizingiti. Lakini labda imani yao kwa Taifa, hasa Serikali, ni ndogo kuliko punje ya mbegu ya mchicha kutokana na sababu mbalimbali.

Nakusihi Kijana kutojificha kama unadhani una uwezo wa kuwa kiongozi kwani Tanzania inakuhitaji (sio lazima iwe kwenye Siasa).

5 comments:

  1. Kwa kweli mimi sio mpenzi wa fikra tuliyonayo Tanzania ya kujivunia eti nchi yetu ni ya watu wakarimu na upole. Tunajua manufaa ya characteristics hizi socially of course (na hata katika diplomasia), ila ni hulka hizohizo ambazo nadhani zinatufanya tusiwe na uimara katika maendeleo. Tokea utotoni tunafundishwa taratibu ya kuwa wanyenyekevu majumbani, mashuleni, mtaani n.k. Dhana ya kusimama, kujitetea na kuuliza maswali kwa wakubwa au wenye mamlaka inapigwa chini. Mwisho wake hata ukija kuwa na watu werevu, wasiopokuwa aggressive mi naona ni bure tupu. Yawezekana nimeingia nje ya mada, ila uwoga wa uongozi kwa wengi wetu nadhani una chimbuko tokea taratibu zetu tunazofundishwa tangu utotoni. Tunahitaji uimara katika maendeleo sasa, na watu lukuki walio aggressive tunawahitaji sasa katika biashara, sayansi, uhandisi na siasa.

    ReplyDelete
  2. hii ni hoja kabambe, sema sasa ugumu wa hili la vijana wenye uwezo, hata wazee kujitokeza linakwamishwa na hivi vyama vya siasa vya sasa. Hoja ya wagombea binafsi limekuwa likijadiliwa kwa miaka sasa, na nia ya watu kadhaa kutaka tuwe na utaratibu wa wagombea binafsi ni hii hii, kukwepa kupitia ujinga mwingi uliojaa vyama vingi vya siasa. Ngoja nitoe mfano, TLP miaka nenda rudi ni Mrema tu ndio mgombea na mtu pekee anayesikia, chama cha UDP ni Cheyo, CUF ni Maalim Seif na Lipumba, yaani hakuna changamoto yoyote huko.

    Tukikumbuka mwalimu alisemaga kuwa mabadiliko halisi hayataletwa na vyama vya upinzani bali ndani ya CCM, na hii ni kweli kwani CCM ya leo imegawanyika, kukiwa na makundi ambayo yamechoshwa na rushwa n.k uliojaa kwenye chama hicho. Hivyo basi, kama CCM ni chama chenye nguvu na wanasiasa wakongwe, basi tuombe mgawanyiko huo utakuwa ni "kuvuja kwa pakacha nafuu ya mchukuzi" kwani vyama vya upinzani wao wenyewe hawajijui.

    Atakayekuwa na muda, atafute clip CNN zinazomzungumzia rais wa Botswana, na kazi anayofanya huko nchini mwake. Mfumo wa siasa tawala ya sasa hivi Tanzania imejaa ushikaji badala ya ufanisi...kama wenye uwezo mpo tunaomba mjitokeze, akina desh desh wameshindwa kazi Tanzania, sitaji majina...hahah!!

    ReplyDelete
  3. by the way, Kalapina anagombea udiwani Kinondoni, I guess pole pole ndio mwendo, vijana ndio hivyo tena na siasa, Bongo Hip Hop & Politics, kazi ipo hapo...haha

    kwa zaidi soma: http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=13745

    ReplyDelete
  4. @ Anon
    Sidhani kama umetoka sana kwenye topic. Kwasababu naamini, kwa njia moja au nyingine, malezi yetu kwenye familia zetu nyumbani ndio hutupa picha halisi ya jamii kwa ujumla. Lakini sidhani tunapaswa kuwa "aggressive"; unaweza ukawaunganisha watu hata kwa kutumia upole na ukarimu wako. Mandela hakuwa anafanya 'fujo' wakati yuko Robben Island. Binafsi nadhani muhimu ni ile vision ya mtu na mpangilio wa utekelezaji (nini kifanyike).

    @ Bahati
    Nimekuelewa na nilijua hautaniangusha! Unadhani kiongozi lazima ajiingize kwenye siasa? Au awe kwenye chama cha siasa? Haiwezekani mtu kuwa mwanaharakati tu?

    ReplyDelete
  5. Heshima yangu kwa Mwalimu ni kubwa sana. Sio heshima ya hyprocrit BLIND YES MAN, ni ule UTU wake. Vile alivyojitoa muhanga kupigania alichakiamini kwa manufaa yake na ya watu wake. Manufaa yake kwa maana alipigania aliloliamini.

    Sio bure kuwa hadi leo hakuna HATA mmoja wa aina yake aliojitokeza. Watu wa aina hii ni nadra sana.

    Wapo viongozi leo hii ambao inasemekana walikwisha kusema maneno kama kiapo kuwa mradi wao wako hai, hata Nyerere asemeje, ujamaa hautajengwa Tanzania. Nao wanaendelea. Ndio maana unaona maandishi yanasema tofauti na vitendo.

    Mimi ni mmojawapo ninayeunga mkono kuwa, tupunguze maneno, tuje kwenye matendo. Vilevile najua kuwa kasi yangu ya matendo ningependa iwe kubwa zaidi. Vitendo sio kugombea uongozi tuu , kuna mengi. Huduma kwa jamii zako, unakoishi, nyumbani kwenu, na kujitolea kwa moyo wote. Uongozi ni wito (calling) na mara nyingi sio kwa kujikweza. Kujikweza kukiwa na uzito, nadhani ndio tunaishia na kutoridhishwa kwani aliejikweza, alijikweza kwa manufaa yake sio yetu. Sasa yeye kwenye malengo yake anakuwa amefanikiwa wakati watu wake hawapo pale yeye alipovukia.

    Kuna sera ambazo zilitekelezwa bila umakini wakati wa awamu ya Mwl Nyerere. Lakini, hadi leo sioni tatizo kwa watu kuishi Kiujamaa na Kwa Kujitegemea. Kuijamaa sio Kiujima. Kiujamaa kwangu ni brotherlyhood, kindugu, kirafiki, kijamii - cooperation. Mnaweza kufanya hivi kwa mlengo wa KIBEPARI vile vile (ulimbikazi mtaji - capitalization). Mnaweza kufanya hivi kwa MLENGO wa Ubeberu vilevile (Uonevu). Lakini hii haina amani. Ujamaa wa Mwalimu ni ile hali ambayo BINADAMU angekuwa PERFECT au awe na LENGO hilo. Pia "Cooperation" au Ujamaa wa 1960s, sio wa 2010. Ila halijabadilika kuwa wanyonge lazima washikamane na waangalie mazuri ya kushikamana ili kuondokana na unyonge na kujikwamua kiuchumi, kuondokana na UJINGA , na maradhi ya MARA kwa MARA. Lazima watu wajifunze kuwa na DREAMS kubwa and kuwa na MOYO kuzifuatilia, BILA kumhujumu mwenzio! Huwezi mhujumu kaka yako uendelee alafu utegemee kuishi kwa amani, HATA siku moja. Ni ngumu haswa pale unapokuta wale baadhi ya "mabwana wakubwa" wanapatwa na woga wanyonge wanapoweza kuwa wamoja wa kweli kweli, sio wa kubabaisha. Ukweli myonge akishikamana na mnyonge mwenzie na wakawa wengi na wakatumia akili, unyonge utaisha na hawatanyonywa tena. Miundo ya serikali zetu ni kunyonya wanyonge - angalia taxation system, uuzaji wa mazao, na matumizi mazima ya pesa za mapato ya serikali utaona wazi kuwa mnyonge anazidi kukandamizwa kutokana na mfumo na pia hulka za viongozi wetu wengi. Hizi challange nyingi za mfumo ni toka enzi za Mwalimu, ila sasa ziko wazi zaidi.

    Uongozi uanze kwenye self assessment, na pia kwenye harakati mbalimbali. Kwa wale kwenye public roles za Kitaifa, ni kazi kubwa zaidi na yenye kuhitaji umakini wa hali ya juu, sio tuu JAZBA (emotions), manake DIRA ni muhimu ili kiwe kitu cha kudumu.

    Lakini vilevile, kwenye mijadala mijadala iwe ya kuelimishana, kusaidiana, na kujengana. Mawazo yakitolewa, yatatekelezwa kama yametafakariwa vema, kuna wakati yatatekelezwa tuu, kwani kilichotoka kinywani, huonyesha ya moyoni na hukamilika pale yanapotekelezwa hata kama sio na mtoa hoja.

    Mwalimu pia alitaka sana kila Mtanzania awe na mwamko wa kisiasa. Hili nadhani limetimilika. Kwenye matendo tuko nyuma bado. Ni vizuri tukijua mapungufu yetu.

    Pia Mwalimu akiwa Mafia kwenye ziara aliwahi kuhoji watu wasiwe na woga wa kuhoji viongozi wao. Alisema hili pale alipowauliza watu waseme matatizo yao wakati wa ziara. Walimwambia HAKUNA matatizo! He knew that was a lie! Akapiga debe watu muongee!! Leo pia inabidi tusiwe waogo manake wengi wetu ni waoga kuongea!


    Tusife moyo, kwani hiyo ndio hatari zaidi.

    ReplyDelete