Miaka miwili iliyopita, mwanahisabati maarufu wa kitanzania Prof. Leonard Shayo alifariki dunia. Msomi huyu alikuwa na ndoto. Ndoto yake ilikuwa ni kuanzisha kijiji cha sayansi na teknolojia nchini (International Village of Science and Technology - IVST) ambacho kingekua kituo kinachokusanya wanafunzi wa kitanzania wenye vipaji katika hisabati na sayansi. Nia haikuwa kuwakusanya tu, bali pia kuwaweka katika mazingira ambayo yangewawezesha kukuza vipaji vyao chini ya usimamizi wa magwiji wa kimataifa katika masomo ya sayansi.
Mchakato wa kuanzisha kijiji hiki aliuanza mwaka 1987, na hadi mwanzoni mwa miaka ya tisini mpango ulipewa heko na jamii nzima ya wanazuoni na hata hayati Mwl. Nyerere 'aliupigia debe'. Ofisi za IVST zilizinduliwa pale AICC Arusha, na mpango ulikuwa kijiji hiki kianzishwe Arusha. Cha kusikitisha mamlaka ya Ardhi ilitupilia mbali ombi la kibali cha kiwanja, kwa sababu mbalimbali ambazo hadi leo hii hazifahamiki. Na huu ndio ulikuwa mwanzo wa mwisho wa ndoto ya Prof. Shayo kuanzisha kijiji hiki muhimu.
Katika muongo huu, ndoto ya Prof. Shayo yaweza kutimia. Kuna mpango mkubwa wa kuanzisha vituo vya sayansi kama vya Prof. Shayo barani Afrika unaosimamiwa na mwanafizikia maarufu kutoka bondeni Prof. Neil Turok. Kupitia chuo alichokianzisha cha African Institute for Mathematical Science chenye makao makuu huko bondeni, Prof. Turok nae ana ndoto ya kujenga vituo kama hivi kila kona ya bara la Afrika ili kusaidia kukuza mafunzo ya hisabati na sayansi. Ndoto yake ni kumpata gwiji wa fizikia/hisabati kutoka Afrika atakayeleta mabadiliko katika sayansi kama aliyoleta Albert Einstein katika karne ya 20. Tanzania ni moja ya nchi ambayo kituo cha AIMS kinatarajiwa kujengwa. Hadi hivi sasa mchakato huu bado upo katika majadiliano.
Tunajua kuwa elimu ya sayansi na hisabati inazembewa na wengi nchini. Ila hii isiwe sababu ya kutohimiza suala hili kwa hali na mali kwa wanafunzi wetu. Nina imani pia, Tanzania yaweza zalisha akina Einstein iwapo tukiwa na jitihada maalumu kusimamia somo la hisabati katika mitaala ya elimu yetu. Kwa wanaosimamia mazungumzo ya mchakato wa kuanzisha kituo cha AIMS Tanzania, msituangushe.
Tuna safari ndefu sana mpaka kuwafikia wenzetu kwenye haya mambo ya hisabati na sayansi (utafiti). Lakini kwa jitihada kama hizi, tutafika tu!
ReplyDeleteNingependa kusikia mipango ya kuwashirikisha watu mbalimbali ambao wanaweza kusaidia..labda baadhi watapata michongo, au kuwapa sababu ya kurudi nyumbani.
Prof. Shayo (RIP) was a visionary!!
ReplyDeleteRemember Erasto Mpemba, of the Mpemba Effect?
ReplyDeletehttp://en.wikipedia.org/wiki/Mpemba_effect
Mambo kama haya ni muhimu kuanza mapema. Kwasababu hata mtu akiwa na kipaji, kama hapati msaada wa kutosha na mazingira yanayofaa kukuza na kukiendeleza kipaji basi atapokipoteza bila kujua.
ReplyDeleteWakati huo huo, ukiacha kukuza vipaji na kufanya tafiti, ni vyema wahusika wakawanoa vijana husika ili wawe wananchi bora -- wenye uwezo wa kuona pale jamii inapohitaji msaada na mabadiliko (na sio kukaa kwenye maabara tu!).