Friday, May 21, 2010

Utoaji mimba

Kuna mambo nyeti ambayo hupaswa kuangaliwa na kujadiliwa kwa utulivu wa hali ya juu. Hatuna budi kujaribu kuweka hisia na "uzoefu" wetu pembeni ili tuweze kupata suluhisho ambalo litasaidia mabinti na dada zetu; bila kusahau vizazi vyetu vijavyo kwa ujumla.

Kutokana na utoto wangu, nimekuja kulielewa na kuanza kulifuatilia suala la utoaji mimba nilipokuwa kidato cha pili. Wakati ule nilikuwa nashangaa: Vipi, Vijana wanaonekana wanashiriki sana kwenye vitendo vya ngono, lakini "matokeo" (ukiacha Ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa) mbona siyaoni? Na akili yangu ilikuwa inaniambia hivi vitu vitatu vina tabia ya kwenda sambamba kwenye jamii zenye desturi kama zetu.

Bahati mbaya watu walionipa mwangaza kwenye mambo yanayoendelea mitaani walikuwa ni Vijana wenzangu vijiweni.

Utoaji mimba... Unashtukia binti fulani anatoweka darasani kwa siku kadhaa halafu akirudi unaona kuna mabadiliko fulani. Ingawa bado nilikuwa kinda, lakini kuna ile sauti kichwani kwangu iliyokuwa inaniambia kuwa vitu haviko sawa kama inavyotakiwa.

Wiki mbili zilizopita Serikali imeamua kuvalia njuga hili suala na kuanza kufunga zahanati na vituo vyote ambavyo hushiriki (kwenye) utoaji mimba. Inaonekana Serikali kama inatumia ile tactic ya kijeshi ya kumshtukiza adui wakati hategemei kabisa kushambuliwa. Lakini tukumbuke hapa tunapigana vita na kuuana wenyewe tu.

Mimi sio mtaalamu wa afya na nisingependa kuhusisha imani za dini kwenye huu mjadala. Kwa kifupi -- kwa maoni yangu binafsi -- nadhani wazee wetu wangejaribu kulivalia njuga hili suala kwa upole kiasi. Kwanza, kuangalia nini hasa ni chanzo cha hizi mimba zisizo na mpangilio. Pili, kujaribu kupunguza haya matukio kwa kutumia elimu na sauti ya utulivu. Tatu, kuwaonya na kuwaambia watu wanaohusika na utoaji mimba kuwa 'tunawaona, tunawajua na tunaamuru muanze kusafisha nyumba zenu!'

Bila kusahau kuwaasa wazazi kuongea na watoto wao kwa uwazi - mabinti na wavulana, pia. Kwasababu inaonekana jamii yetu bado ina ile soni ya kuongelea mambo ya ngono na madhara yake.

Nisingependa kuwapotezea muda wenu kwasababu nina uhakika hamtajifunza jipya kutoka kwangu. Kwahiyo, nawaasa wale ambao wanasomea haya mambo, kuyafuatilia au kufuatilia nchi ambazo takwimu zao kwenye mambo kama haya ni nzuri, kutupa ujuzi na maoni.

Natumaini sauti zetu zitawafikia wahusika, kwasababu hili jambo ni nyeti mno na linahitaji kuguswa kwa utulivu kama tunavyotoa uchafu kwenye mboni za macho yetu.

7 comments:

 1. This comment has been removed by the author.

  ReplyDelete
 2. On similar topic, nimesikia kuna mchakato unaoendelea katika baadhi ya vitongoji (mf. Mlandizi) wa kuwachoma sindano za uzazi wa mpango wanafunzi pamoja na watu wazima. http://en.wikipedia.org/wiki/Depo-Provera

  Ingawa tunataka kupunguza mimba holela, je hili jambo ni sawa kwa wanafunzi? (haitachochea kusambaa kwa STDs kweli?) On the other hand, contraception methods kama hizi zisipohimizwa, suala la utoaji mimba si nalo litadumu?

  ReplyDelete
 3. Hapo ndipo kazi ilipo -- kujaribu kuwa na uwiano mzuri wa elimu (kusambaza taarifa) ya uzazi na magonjwa ya zinaa. Wakati huo huo tunatakiwa kuamua ni umri gani hasa ambao wanafunzi wanatakiwa wapewe hizi taarifa; tukizingatia umri ambao vijana wanapevuka na kuanza kujaribu vitu wanavyosikia mitaani.

  Nadhani kuwa wawazi kwa wadogo zetu itatusaidia kwa kiasi kikubwa. Hatuwezi kuiga kila kitu kutoka Magharibi, lakini hatuna budi kujaribu kuangalia wanachofanya. Kwa mfano, Uholanzi ni nchi inayojulikana na kuwa na 'rate' ndogo sana ya mimba za wanafunzi. Ukiangalia kwa juu juu unaweza ukasema matatizo kama haya lazima yatakuwa makubwa (kwasababu ya vitendo vya biashara ya ngono n.k.) kuzidi Tanzania (ambako mambo haya ni "mageni"). Lakini ni kinyume kabisa... Na kinachowasaidia wenzetu ni kuwa wawazi na kuwapa taarifa mapema sana wanafunzi.

  Unaweza ukasema mambo haya hayatokei kwenye jamii yetu. Lakini Serikali inapotoa tamko kali kama hili ndio unakuja kugundua jinsi tatizo lilivyokuwa kubwa!

  ReplyDelete
 4. Utoaji mimba haujasaidia nchi yeyote.Ni uhuaji tu ambao hauna maana yeyote na haupaswi kuvumiliwa.Siongelei hii kwa misingi ya kidini tu la hasha,lakini najaribu kufikiria kama wazazi wetu huko nyuma wangetoa mimba zetu labda tusingekuwa na nafasi ya kuandika maoni hapa!

  "Live and let live"....kama wewe unaishi basi wape nafasi na wengi ambao umeshiriki kuwatengeneza waishi...kama kijana ameamua kushiriki kwenye vitendo vya ngono katika umri mdogo au akiwa mwanafunzi ajue fika kuwa mimba ni moja ya matokeo na kama kijana huyu ana nafasi ya kuzaa basi na aachwe azae maana atakuwa amejifunza jambi kubwa kuliko kuamua kuaa kiumbe ambacho hakina hatia.

  Utuamiaji wa sindano,vipandikizi na njia nyingine za kisasa za uzazi wa mpango umekuwa na madhara makubwa mno kwa watumiaji.Dada na mama zetu wanakumbwa na matatizo kadha wa kadha na ningeshauri tujaribu kufanya utafiti kabla ya kuamua kutumia hizi njia!

  ReplyDelete
 5. @ Anon, nitazungumzia aya ya mwisho kwanza.

  Kweli njia za uzazi wa mpango ni nyingi na sio kila msichana au mwanamke zinamfaa. Nimepitia makabrasha ya uzazi wa mpango wakati nakua - kinachotakiwa kufanywa ni kufanya blood tests kabla ya kuamua njia ipi inakufaa. Kila mtu ana hormonal make up yake. Na kuna dada zetu ambao wana hormonal imbalance. Sasa je, ni wangapi wanalijua hilo? Ya kwamba, kabla ya kuanza kubugia vidonge fulani lazima ufanye blood tests ili kujua njia au vidonge vipi vinakufaa.

  Kuhusu maoni yako kwenye aya mbili za kwanza, ningependa kuuliza: Unaamini maisha ya binadamu yanaanza wakati gani? Baada ya fertilization (immediately)? Baada ya miezi au wiki kadhaa (baada ya tendo la 'ndoa')?

  Nielewe ya kuwa sina msimamo sana kwenye haya mambo na ninataka kujifunza kutoka kwa wengine. Na ninawaasa vijana wenzangu "kutuliza majeshi." Muda upo mwingi tu!

  Vipi kuhusu wale wanaobakwa? Ni sawa kutoa mimba ili kuokoa maisha ya mama?

  ReplyDelete
 6. najaribu kutafakari zaidi bila kuwa mnafiki... sitaki kusukumwa na maadili bali uchambuzi na hali halisi, nikitazama ushahidi huu... 'Unfortunately only 33 percent of boys and 50 percent of the girls reported using condoms in their first sexual encounter: “About one in 10 students who have had sex did not know whether a condom had been used. A similar pattern is seen for condom use at last sex.” halafu tena 'in South Africa, 23% of females had their first sexual experience with someone much older than themselves. The data suggests that much early sexual experience is conducted in contexts where there are such marked power and maturity differentials that manipulation must be considered an important determinant of early sexual experience'. Binafsi nimeshiriki katika utafiti wa hali za vijana Lesotho, na zaidi ya 40% ya wasichana wanasema their first sex was a rape... katika hali hii na ushahidi hapo juu ni kuwa asilimia kubwa ya wasichana hufanya ngono mara ya kwanza bila ridhaa yao. katika hali hii wengi hupata mimba wasizotarajia na mbaya ni kuwa kina baba wanawatelekeza, wasichana wanafukuzwa shule na nyumbani pia ilhali wanaume wanapeta. Hawakupanga kupata mimba. msichana anapobakwa hapangi kupata mimba. Hivi unamsaidiaje binti kama huyu? Azae tu ili ajifunze? Kwanini mtu ajifunze kwa makosa ya mtu mwingine? Angalau wanaume wangekuwa wanabeba mimba wangeelewa.
  Binafsi sioni tatizo la safe abortion, si kwa sababu ya kuiga umagharibi bali katika hali ambayo inalazimu kumsaidia mtoto wa kike? Vipi kama inalazimu kufanya abortion ili kuokoa maisha ya mama! bahati mbaya tunagubikwa na mitazamo ambayo inang'ang'ania maadili bila maarifa.Najua watu wa mrengo wa pro-life wanachukia sana lakini huwezi kupingana na ukweli na hali halisi. leo nilikuwa nasikiliza presentation toka mtu wa Ministry of Health Tz hapa Kampala, huwezi amini kuwa mahitaji ya supplies za reproductive health ni 9bln Tsh lakini pesa ambayo imekuwa allocated ni 2bln Tsh, hii ni pamoja na contraceptives na family planning methods... sasa jiulize ni wangapi hasa vijana hususani wanapata? Inawezekana kuwa ni kweli utoaji mimba haujasaidia? lakini mbona inafanyika tena sana na kwa kificho ambayo ni hatari zaidi? siungi mkono kuwa hili jambo lifanyike kiholela lakini lazima kujenga mazingira ambayo yatafanya utekelezaji wake ufanyike kwa umakini na usalama. hata tukijidanganya bado itaendelea... mbaya zaidi tunajifunika shuka la maadili na kuziba nyuso tusione ukweli... KWELI NDIO ITATUWEKA HURU

  ReplyDelete
 7. Wakati nafikiria kuandika hii makala ili kuchokoza mawazo ya watu, nilikuwa naombea utokee mjadala ambao utafundisha wengi (hasa vijana). Tovuti niliyoiambatanisha hapo juu (kwenye post) inakupa picha ya mambo ambayo hayaongelewi kabisa; ni mwiko kujadili -- lakini watu wamepewa nafasi na wameamua kutoa ule ukweli wa mambo yanayofanyika kwenye giza.

  Kwahiyo, nashukuru Ndg Shakim kwa kutuletea facts. Nilipata fursa ya kuangalia documentary moja (ya Bondeni) ambayo inasema katika kila wasichana wanne, mmoja amebakwa angalau mara moja! Inasikitisha lakini ndio ukweli -- hatuwezi kuyafumbia macho haya mambo na kujifanya kila kitu ni shwari.

  Ninachojaribu kusema ni hiki: Kama Shakim alivyosema hapo juu, ukweli ndio utatuweka huru. Ongeeni na watoto wenu vizuri. Jiulizeni kwanini wanakimbilia kutoa mimba kiholela? Hatari?

  Na kwa upande mwingine, Wizara ya Afya kukurupuka na kuamua kufunga hizi zahanati zote, nadhani hii italeta madhara zaidi kuliko manufaa kwa jamii.

  ReplyDelete