Friday, March 5, 2010

ZINDUKA na Bongo Flava...

Zinduka ni mpango wa kuweneza ufahamu juu ya janga la malaria kwa nia ya kutokomeza ugonjwa huu. Mpango wa 'Zinduka' unatumia sanaa ya muziki kuhamasisha wananchi ili kujiunga katika kupigana na malaria na kujenga Tanzania iliyokuwa haina malaria, kwani 'inawezekana'. Sasa sijui ni mikakati ipi hiyo serikali ilinayo ya kutokomeza malaria kabisa kama bado kuna mazingira kibao yanayochochea kuzaliana kwa mbu, swali hilo kwa walengwa wakuu. Malaria = Umasikini au, sasa kama tunakubaliana na hoja hiyo, hivyo lipi tulishughulikie kwa kasi, malaria au umasikini ambao unauchochea, ni wazo tu.

Mpango huu umenifurahisha jambo moja, na hilo ni kutumia muziki wa Bongo Flava katika kujaribu kuhamasisha na kuelimisha jamii katika kupambana na malaria. Nyimbo hii inanikumbusha nyimbo ya 'We Are The World' kwa ajili ya Ethiopia na ya hivi kitambo kwa ajili ya Haiti. Nimependa sana wazo hili la uhusishwaji wa vijana katika mpango kwa njia ya bongo flava ambao unasikilizwa na wengi, kwani vijana na sisi tunaadhirika na janga hili la malaria. Nadhani serikali inabidi ihusishe vijana zaidi katika maswala ya kijamii, kwani sisi ndio wajenzi na waadhirika wakuu wa magonjwa na umasikini. Tanzania bila malaria haiwezekani mpango umasikini upunguzwe na makazi ya watu kuboreshwa, lakini bila hivyo tunajaza maji kwenye gunia.

Ningependa kusikia mawazo kwenye upande wa uzuri wa muziki wenyewe , kama kweli unamvuto na unaweza kuvutia watu na kuwahamasisha au hauna mvuto kihivyo. Mimi nadhani utunzi na utengenezaji wa nyimbo yenyewe ungeweza kuwa mzuri zaidi. Lakini wanasema, kila safari ndefu huanza na hatua moja, na hivi ndivyo tunaanza hivyo hongereni mwanzo mzuri.2 comments:

 1. Hizi kampenseli mi naona ni kupoteza muda, na kunufaisha wachache (tazama purukushani kati ya waandaaji na MR II). Waandaaji wanaangalia ni namna gani wanaweza kutoka na chochote ambacho ni fedha ya wafadhili. Sidhani ni mwananchi gani ambaye hafahamu namna ya kujiepusha na mbu wa malaria (kukata vichaka, neti, nk). Malaria ipo, na imekuwepo miaka elfu kadhaa, ni budi wananchi kuhamasishwa kwenda hospitali mapema kwa ajili ya matibabu. Hapa linakuja jambo lingine, umaskini wetu ukizidi kukithiri basi tutaendelea kufa kwa malaria. Kwani tusipokuwa na hospitali za kutosha zenye wauguzi na madawa ya kutosha (zilizothibitishwa na WHO) malaria itatuangamiza.

  ReplyDelete
 2. Nafikiri ni wazo zuri kwasababu ujumbe utawafikia wahusika ambao wengi ni vijana. Ujue kuwa na takwimu kama zetu ambazo zinaonesha ugonjwa kama malaria, ambao ni rahisi kujilinda nao au kupona, kuathiri watu wengin sio jambo la busara. Ukizingatia dawa zipo, zana (neti) za kuzuia kung'atwa na mbu zinapatikana.

  Sasa mtu anaposhindwa kujilinda tu; au kufuata maelekezo rahisi ya kuponya malaria ujue kuna kitu kinakosekana. Tuangalie wenzetu ambao kipindupindu mara ya mwisho kukiona kwenye nchi zao ilikuwa miaka 1960. Na ilikuwa sijui ni watu wawili watatu tu - sio milipuko tuliyozoea kusikia nyumbani kila masika.

  Naelewa kuwa parasite ana-'evolve' na kufanya mambo yawe magumu. Lakini, kufuata maelekezo ya kunywa dawa sio ngumu, au?

  Huu usiwe mwanzo na mwisho tu. Vitu kama hivi vinahitajika kila mwaka nadhani.

  ReplyDelete