Tuesday, April 20, 2010

Uchawi na Ushirikina

Picha za vitendo vya ushirikina na uchawi nilizoziona kwenye blogs mbalimbali wiki iliyopita bado zipo kwenye mawazo yangu. Kuandika makala mara nyingi huwa ni jambo rahisi kwangu, muda tu ndio kitu ninachohitaji. Lakini nashindwa...Sijui nianzie wapi; sijui niandike nini; na wala sijui dondoo za makala ziwe vipi. Napata hisia ngeni -- hasira, simanzi na nadhani ubongo wangu unashindwa kutoa ujumbe ambao nataka uwafikie Watanzania wenzangu.

Tumemkosea nani kwenye dunia hii? Je, tunastahili kushuhudia vitendo vinavyoendelea kufanywa na Watanzania wenzetu? Akili changa za wadogo zangu hazipaswi kuanza kutafakari ushirikina unaofanywa na wanajamii wenzetu. Vilio vya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi vinatua kwenye ngoma safi za masikio ya watoto wetu. Mboni nadhifu zinapokea mwanga unaobeba taswira ambazo...Ah! Nalengwa na machozi.

Viganja vyangu nahisi vimekuwa vizito na siwezi kuandika kwa kasi ya kawaida. Nawakumbuka ndugu na rafiki zangu wenye ulemavu wa ngozi na naamua kupiga moyo konde kukemea upumbavu, ujinga na fikra potofu zilizopo kwenye vichwa vya Watanzania -- sijui ni wachache au wengi.

Ripoti yenye takwimu kuhusu tabia na desturi za Waafrika bila shaka ilitushtua wengi! Sidhani kama takwimu zilizotolewa kuhusu imani za ushirikina na uchawi Tanzania ni sahihi. Lakini hata kama wangesema ni asilimia moja tu ya Watanzania, bado ningejiuliza maswali mengi sana.

Miaka iliyopita tulikuwa tunaongelea suala la ushirikina na uchawi kwa utani. Ilikuwa ni kichekesho tu pale tuliposikia timu fulani imeingia uwanja wa Taifa kwa kuruka ukuta. Au mashabiki kuchimbia hirizi kwenye viwanja vya mpira. Na hata hatukushtuka pale watu walipoamua kufukia vichwa vya mbuzi.

Wale ambao tulikuwa 'tumelala' tuliamshwa na kelele za vilio vya wazee Shinyanga, Mwanza na Mara mwanzoni mwa miaka ya 2000. Vikongwe (ambao walikuwa hawana jinsi, bali kuwapikia chakula wajukuu na vitukuu vyao kwa kutumia kuni zinazotoa moshi) walipigwa mapanga bila huruma. Angalia tulipofika sasa.

Itachukua miaka mingi sana kusafisha jina la nchi yetu.

Natamani haya yote yangetokea kwenye ndoto...

7 comments:

  1. Hata mimi nashindwa kuelewa. Tatizo lipo wapi.. umaskini, tamaa za watu kutajirika haraka, au ujinga?

    Serikali imechukua hatua zake lkn sidhani kama wataweza kufanikiwa bila msaada wa kila mwananchi. Tuanzie wapi...

    ReplyDelete
  2. Hii kitu ni process tu. Maendeleo, yakija upuuzi wa ushirikina utapotea tu.

    ReplyDelete
  3. tamaduni ni kitu kigumu sana kubadilika, kama imani katika dini, hisia ya kupenda kutoka mtu mmoja kwenda kwa mwingine, hivi vitu vinakuwa na mizizi ya ajabu.

    Sisemi tamaduni zetu za kiafrika ni tamaduni zilizojaa na ushirikina, hapana, lakini sidhani tunaweza tenganisha imani hizi za giza na baadhi ya mila zetu moja kwa moja. Maendeleo yanaweza punguza lakini hayawezi badili hizi imani, hasa ukizingatia watu hurithishwa hizi imani.

    Inasikitisha kuwa mambo kama haya yamezidi shamiri lakini ndio hivyo tena, umasikini na elimu duni, lakini mwisho wa siku ndo mila tena..kazi ipo hapo

    ReplyDelete
  4. Kuhusu mila na desturi zetu, mmenikumbusha majadiliano ya Obama na mwanahistoria mmoja wa Kenya (kwenye kitabu chake).

    Tunapenda kukumbatia "mambo yetu" na kuna wakati mtu kutoka nje anapokuja na kutuambia msifanye hivi au vile - kutokana na sababu mbalimbali - tunakuwa wakali. Na hii hutokea bila hata kutofikiria kwa makini maoni ya 'mgeni'.

    Dunia imebadilika na inaendelea kubadilika kwa kasi. Makabila yetu yalikuwa na mila na desturi ambazo sasa hivi sote tunajua kuwa baadhi zilikuwa sio nzuri. Mfano mzuri ni tohara kwa mabinti zetu. Serikali yetu nadhani ilivalia hili suala njuga na mambo yamebadilika.

    Kwa kifupi, inabidi tujitahidi kupanua wigo wa mawazo yetu. Kama Serikali na sekta husika itabidi zitumie "nguvu", basi iwe hivyo. Tusikilize maoni ya watu na tuangalie, je, ni kweli? Kuna faida za kuacha baadhi za mila zetu na kuzisahau kabisa?

    ReplyDelete
  5. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete
  6. Naona mada inazidi kunoga. Ningependa kurejea kwenye nilichosema kabla. Swala la watu na mila na desturi zao ni kama mlevi wa pombe au mlevi wa madawa ya kulevya wa miaka mingi. Dini ni kitu kingine, kwani hapo sasa kunaingia swala la imani, na imani ikishaingia tu, ni ngumu sana kuitoa. Anayebisha ajiulize ni vipi mtu anaweza kujilipua mwenyewe ili kuuwa wengine kwasababu ya mungu, jibu ni Imani.

    Sasa basi, watu wanaodhani kuwa kuleta sheria mpya ambazo zinatafsiriwa kama tamaduni za kigeni, kuja kusaidia kuondoa mila, desturi na imani za watu ni jambo gumu sana. Kitu ambacho umekuwa nacho kwa miaka na miaka, si rahisi kuacha tu ghafla, na hasa kama kinahusiana na imani ya mtu. Leo hii mtu ajaribu kukulazimisha kuanza kutumia mkono wa kushoto (kama wewe ni wakulia) kuandikia, kulia, n.k itakuwa vigumu sana.

    Sasa basi, je kama ni ngumu hivyo tuache mila na desturi zilizopitwa na wakati ziendelea kumea kwenye jamii zetu, jibu ni hapa. Mfano, hilo swala la tohara linawashinda watu kwasababu njia ya kulazimisha watu kuacha kitu ambacho wamekizoe kufanya tangia miaka na miaka sio rahisi. Wengi wao wanaokwenda vijijini na polisi ndio wanaharibu kabisa, kwani badala ya kukaa na kujadiliana nao, wao huwasulubu na wao (wahusika) wanaona Serikali ndio adui na hata kujenga chuki juu yake, sasa tunategemea wao wataacha hiyo mila tukiwashinikiza badala ya kujadili nao huku tukiwaelimisha.

    Swala la tohara lilikuwa na sababu nzuri tu, lakini sasa namna ya kufikia hilo lengo ndio hapo kukawa na mapungufu. Mila na desturi ya tohara ilikuwa na lengo la kusaidia kulinda ndoa, kwa kuchunga wanawake wasijikute wanacheza nje, sema sasa mila hii haikuwabana wanaume (tatizo namba mbili). Niya ya mila hiyo ilikuwa nzuri sema utekelezaji ndio ukawa sio sahihi.

    Kwenye swala la tohara nadhani ni bora watu wangeelimishwa vizuri adhari zake, na kujaribu kutafutiwa njia mbadala la kuhakikisha ndoa zinadumu, kwa mfano. Badala ya tohara ili kuhakikisha mwanamke hawachezi nje, mila ya wanawake kupelekwa unyagoni ingesisitizwe zaidi. Hapo hapo na mila ya wavulana kupelekwa jandoni nayo ingetiliwe mkazo, hivyo basi masomo ya huko ndio hayo yatakayo saidia kujenga jamii njema, kuliko ukeketwaji.

    Sheria hizi za serikali ni sheria mpya ambazo nyingi zinaonekana kama adui kwa waliokula chumvi nyingi na mila zao. Mila na dini bwana, hivyo vitu viwili vikishamshika mtu, hata ikapitishwa sheria ya kunyongana, watu watajitoa mhanga kutetea mila zao.

    Swala la uchawi nadhani halitaisha kwa sheria za serikali, nadhani kuna umuhimu ya elimu shirikishi kati ya wadau (serikali) na wahusika (wachawi wenyewe) na wananchi ambao ndio waadhirika wa mambo hayo.

    Umasikini nao unachangia, when people are desperate, tow things are very likely to happen. For one, people can become very creative to get themselves out of their unfortunate/ desperate situation or people can do the unthinkable, like witch craft. Life gets tougher, crime goes up, "weirdos" in the society multiply, lets all remmeber the days of Mr. Ruksa, Mwinyi..I bet you things like this were there but with life taking a turn for the worst for many Tanzanians, then things like this have become more visible and more constant than usual. Taking about being an entrepreneur, well there you go, witchcraft is business and just like being a hitman

    In conclusion, the guy was an actor before, but that didnt pay bills am guessing, but witchcraft is, now that should say something. There must be a demand thats why he is where he is, now what does that say about our society. Jamani, malaya wanazidi shamiri mitaani kwasababu wanaume wafuska nao wamejaa mitaani pia, biashara mnunuzi la sivyo mtaji unafilisika na duka linakufa, au mnasemaje...kazi kwenu...

    ReplyDelete
  7. Kazi ipo! Kama ulivyosema, binadamu tunaogopa sana mabadiliko na linapokuja suala la imani...hata wana mazingaombwe wanaweza kuwa 'viongozi wa dini' na tukakubali kuwa wafuasi.

    Mchangiaji mmoja amegusia maendeleo (ila sijui anazungumzia maendeleo ya aina gani haswa), labda yanaweza kufungua mawazo yetu. Mi' nadhani ni kuelimisha tu kwa lugha ya upole ndio inaweza kupunguza. Lakini, imani zao si zitawafanya "waogope" kufuata wanayofundishwa? Kazi ipo...

    http://www.youtube.com/watch?v=EWwFVfd9kY8

    Kuna baadhi yetu -- wasomi -- ambao wanakataa kukiri kuwa tuna tatizo kama donda ndugu na kuamua kushambulia vyombo vya habari vya Magharibi (kama hivyo hapo juu). Kwa maneno mengine, badala ya kujaribu kutafuta suluhisho wanaamua kujibizana kuhusu 'research methods' za hizi ripoti chache tunazoziona..."Wanatudharau na wanataka kutudhalilisha" ndio wanavyodai. Tufumbue macho jamani; tusilikimbie tatizo!

    ReplyDelete