Monday, April 26, 2010

'Flying vaccinator' - mbu mueneza chanjo

Picha kwa hisani ya National Geographic*

Kuna baadhi ya tafiti ambazo zinasisimua, ilihali uwezekano wake wa kuzaa matunda katika mazingira ya sasa ni mdogo. Hivi majuzi tu, wanasayansi nchini Japani wamefanikiwa kumtumia mbu kama chombo cha kusambaza chanjo dhidi ya mdudu anayesababisha Leishmaniasis. Tunajua jinsi tulivyopata chanjo utotoni; mara nyingi ilitubidi tuvumilie kudungwa sindano zenye dawa ya chanjo dhidi ya magonjwa hatari kama polio, hepatitis, kifua kikuu n.k. Katika orodha hii, yanakosekana magonjwa kadhaa (kama malaria) ambayo bado haijapatikana chanjo mahususi, kwa sababu kadhaa. Sababu kubwa ni changamoto ya kisayansi kutengeneza chanjo yenyewe, na pia gharama kubwa ya usambazaji itakayojitokeza iwapo chanjo hiyo ikipatikana.

Wajapani wamekuja na ujuzi ambao kinadharia unaweza tatua tatizo la usambazaji wa chanjo. Wameweza kumtumia mbu kusambaza dozi ya chanjo kila atakapokuwa ananyonya damu (hapa walitumia panya). Walichofanya ni kumbadili mbu maabarani ili aweze kutengeneza dawa ya chanjo dhidi ya Leishmania ndani ya gland zinazotengeneza 'mate' (mbu hutema 'mate' yake kabla ya kunyonya damu ili kuzuia damu kuganda). Wameweza kupima muongezeko wa antibodies kwenye panya waliong'atwa na hivyo kinadharia kufanikisha chanjo.

Je, si itakuwa 'kali' pia tukiweza kutumia mbu kusambaza chanjo dhidi ya malaria na sio mdudu mwenyewe?

Matokeo ya utafiti huu hayako kamili, kwani bado hawajapima uwezo wa chanjo hiyo kupunguza maambukizi ya ugonjwa wenyewe, ila ni tafiti pekee na ya kwanza kuweza kutumia mbu kwa namna hii. Je tutaacha kutumia sindano hapo mbeleni? Je utakubali mbu kama hawa watumiwe kusambaza chanzo za malaria hapo baadaye? Kuhusu dozi je - ukingatwa mara 1000 na mwingine mara 50? Hapa kengele ya maadili na kanuni (ethics) za sayansi inaendelea kulia.

* http://ngm.nationalgeographic.com/2007/07/malaria/finkel-text

3 comments:

  1. Hii kali!

    Makala ilivyoanza..nikaanza kujiandaa kuchoma moto chandarua changu! Sasa, lini tuanze kuchoma vyandarua vyetu moto; ili kuepuka haya magonjwa?

    Hii makala imenikumbusha kile kipindi cha Chaaaaz Hillary "Habari Nyepesi Nyepesi".

    ReplyDelete
  2. what about patient consent? cool, but un-workable

    ReplyDelete
  3. Kweli itakuwa ngumu kufanikiwa. Lakini muhimu ni lile wazo la kutumia mdudu kusambaza au kutoa chanjo. Labda huu utafiti utafungua mawazo yetu na kuanza kuangalia uwezekano wa kuwatumia wadudu wengine ambao hawaenezi magonjwa ili kueneza chanjo.

    ReplyDelete